Halmashauri ya manispaa ya Temeke imepata mstahiki meya mpya baada ya uchaguzi uliofanywa na baraza la kwanza la madiwani katika Manispaa hiyo.Baraza hilo kwa pamoja lilimchagua diwani wa kata ya Kibondemaji Mheshimiwa Abdallah Said Mtinika kuwa meya mpya wa Manispaa hiyo, akichukua nafasi ya mh.Abdallah Chaurembo ambaye kwa sasa ni Mbunge wa jimbo la Mbagala.
Akiongea baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi huo,mh.Mtinika alisema kuwa baraza lake la madiwani ambalo ataliongoza halitakuwa la mazoea na badala yake atafanya kazi kulingana na ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
"Nitahakikisha naifanya manispaa hii kuwa ya kisasa na yeyote ambaye anadhani kuwa kutokana na umbo langu kuwa dogo sitoweza kuifanya kazi hii atakuwa amekosea"Alisema Meya huyo.
Aidha katika uchaguzi huo pia diwani wa kata ya Kurasini Mheshimiwa Arnold Emmanuel Peter alichaguliwa kuwa Naibu meya wa Manispaa hiyo.
Awali akimkaribisha Meya huyo Mkurugenzi wa manispaa ya Temeke Ndugu Lusubilo Mwakabibi, aliwaasa madiwani hao kuheshimu na kutekeleza maagizo kutoka kwa Mstahiki meya kwa kuwa ndiye aliyechaguliwa kwa wakati huo.
"Nataka niwaambie wakuu wangu wa Idara hii ni mamlaka kamili na tufanye kazi kwa ushirikiano na ili kuifanya manispaa yetu kusonga mbele" Alisema Mkurugenzi .
Baadhi ya waheshimiwa madiwani wakila kiapo cha maadili katika ukumbi wa mikutano Iddy Nyundo.
Jumla ya madiwani 35 walipiga kura kumchagua Mstahiki meya na Naibu meya na kabla ya hapo madiwani 23 kutoka kata za manispaa hiyo walikula kiapo cha utii kuanza majukumu yao ya udiwani.Manispaa ya temeke ina jumla ya kata 23 ambapo madiwani wakuchaguliwa jumla yao ni 23,madiwani wa viti maalum 8,wabunge wa kuchaguliwa 2 pamoja na wabunge viti maalum 3 ambao wanaunda Baraza hilo lenye jumla ya madiwani 36.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Katibu tawala mkoa wa Dar es salaam,katibu tawala wa manispaa ya Temeke pamoja Afisa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU).
Manispaa ya Temeke inapatikana mkabala na uwanja wa Taifa katika makutano ya barabara ya Mandela na Taifa.
Anuani ya Posta: P.O.Box 46343 Dar-es-Salaam
Simu ya Mezani: +255 22-2928132
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: temeke@temekemc.go.tz
Hatimiliki©2018. Halmashauri ya Manipaa ya Temeke