Mkuu wa wilaya Temeke Mheshimiwa Godwin Gondwe amemtaka mkandarasi wa kampuni ya SINOHYDRO inayotengeneza barabara ya mwendokasi(DART) awamu ya pili kuhakikisha anafanya kazi hiyo kwa thamani halisi ya fedha.
Mkuu huyo wa wilaya ameyasema hayo alipokuwa akikagua baadhi ya maeneo ya mradi huo ambapo aligundua kasoro nyingi ikiwemo nyufa zilizoanza kujitokeza katika barabara hiyo na vituo vya mabasi katika mradi huo.
Mhe Godwin Gondwe akiwa na kamati ya ulinzi pamoja na wataalam wengine wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa barabara ya Mwendokasi.
"Kwa taarifa nilizonazo ninyi viongozi wa hii kampuni ya SINOHYDRO mnawarubuni vijana wetu waliopo maabara wakatae matokeo rasmi ya maabara na wakikataa mnawafukuza kazi".Alisema Gondwe
Kwa upande wake Meneja mradi wa TANROADS,Injinia Barakael Mmari alimuhakikishia mkuu wa wilaya kuwa atahakikisha anafuatilia na kuwaandikia kwa maandishi mkandarasi huyo.
Akiwataja kwa jina moja moja Mkuu wa wilaya aliwataja Bw.Ten,Yang na Duo kuwa ni miongoni mwa wanaojaribu kuhujumu mradi huo kwa kufanya kazi hiyo chini ya kiwango na kushawishi wataalamu wa maabara kutoa matokeo ambayo si sahihi.
"Siwezi kuona mradi mkubwa ambao Mh.Rais Magufuli anatoa pesa nyingi unahujumiwa halafu mimi nipo hapa,siwezi kukubali Temeke".Alisisitiza Mkuu wa wilaya Temeke.
Mkuu huyo wa wilaya amemtaka Mkandarasi huyo kufuata sheria na taratibu za mkataba zilizowekwa na ameonesha kutoridhishwa kwake na kasi ya ujenzi huo ambao alisema hana uhakika kama utakamilika kwa wakati na ubora unaotakiwa.
"Madhara ya haya tutakuja kuyaona baada ya miaka 10 au 20 mbele,watu watakufa hapa,magari yataanguka watasingizia magari mabovu kumbe barabara ndio mbovu,na huku ni kumuhujumu Mh.Rais."Alibainisha Mh.Gondwe
Mwonekano wa kipande cha ujenzi wa barabara ya Mwendokasi Mbagala.
Manispaa ya Temeke inapatikana mkabala na uwanja wa Taifa katika makutano ya barabara ya Mandela na Taifa.
Anuani ya Posta: P.O.Box 46343 Dar-es-Salaam
Simu ya Mezani: +255 22-2928132
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: temeke@temekemc.go.tz
Hatimiliki©2018. Halmashauri ya Manipaa ya Temeke